📌NA DEVOTHA SONGORWA
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge amewataka
wakazi wa Mkoa huo kuendelea kuwa watulivu wakati huu ambapo Taifa
lipo katika maeombolezo ya siku saba kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu
ya Tatu Benjamin Mkapa.
Dk. Mahenge amesema hayo
wakati viongozi mbalimbali wa serikali wakitoa heshima zao za mwisho zoezi
ambalo linafanyika kwa siku tatu kuanzia jumapili iliyopita likitarajiwa
kukamilika leo jumanne katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Amesema kwamba katika uongozi
wake alikuwa na mchango mkubwa katika Mkoa wa Dodoma pamoja na nchi nzima kwa
kuanzisha Mamlaka na Taasisi mbalimbali kwa lengo la kulipatia Taifa maendeleo.
“Tutaendelea kuenzi vision
aliyoianzisha alipambana kadri anavyoweza akiwa madarakani kwa kugusa kila
sekta naamini alitamani kuona Tanzania inakuwa tofauti ikiwa mikononi mwake
hakuwa msiri alipenda sana uwazi na ukweli hata ukikosea hakunyamaza kwa sababu
alitaka kuona kila mmoja anatenda kadri ya majukumu yake kw anafasi anayoitumikia
tumepoteza mtu muhimu sana”alisema Mkuuu wa mkoa wa hapa.
Akizungumzia uanzishwaji wa
TASAF aliongeza “Marehemu Mkapa yeye ndiye aliyeanzisha Programu za TASAF
tulikuwa na Tasaf ya kwanza, ya pili na sasa tuna ya tatu kwa sababu hakuwa
tayari kuona wananchi wanaishi katika hali ya umasikini uliokithiri na ni moja
ya vita ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kupiga vita maradhi,
ujinga na umasikini na alitembea katika nyayo hizo na sasa tunaona Kaya nyingi
masikini walau wanamudu mahitaji yao ya msingi”aliongeza Dk. Mahenge.
Amebainisha kwamba mengine
amabyo atakumbukwa kwayo ni kuanzisha Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) Mamlaka ya
Mawasiliano (TCRA) Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati
na Maji (EWURA) Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA)
Aidha ameeleza kwamba wakati
wa uhai wake ,Mkapa atakumbukwa kwa mfumuko wa bei za bidhaa kutokupanda mara
kwa mara, migomo ya vyombo vya usafiri wa umma na kuwahimiza watu kufanya kwa
kazi kwa bidii akiesema mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe.
Katika nyanja ya tasnia ya
habari aliweka bayana kwamba katika utendaji wake hakuiacha tasnia hiyo muhimu
kwa nchi akipambana kutetea uhuru wa vyombo vya habari ambapo katika uongozi
wake kulifunguliwa vyombo vya habari ambavyo hutumika kama daraja la maendeleo
ka taifa lolote lile duniani.
“Tusisahau kwenye vyombo vya
habari yeye kama mwanahabari na msomi alileta mageuzi makubwa sana
alitetea uhuru wa habari hata kuanzishwa kwa TV nyingi zilianzshwa katika
utawala wake mimi nilikuwa nje ya nchi kwenye masomo yangu lakini nilishuhudia
mambo makuba aliyoyafanya hatutamsahau”alihitimisha Dk. Mahenge.
Hayati Benjamini William
Mkapa alizaliwa Novemba 12, 1938 mkoani Mtwara na alifariki usiku wa kuamkia
julai 24 mwaka huu baada ya kupata mshutuko wa Moyo wakati akipatiwa matibabu
ya maradhi yalkiyokuwa yakimsumbua jijini Dar es salaam.
Amewahi kushika nyadhifa
mbalimbali za kisiasa na uongozi ikiwemo Urais kwa Awamu ya Tatu kuanzisha
Novemba 23 1995 hadi Desemba 2005 alipong’atuka madarakani. Wakati wote huo
alikuwa pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
0 Comments